Pakistan: Imran Khan amehukumiwa kifungo cha miaka 14 jela kwa kesi ya ufisadi
Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan, Imran Khan, amehukumiwa kifungo cha miaka 14 jela kwa kesi ya ufisadi ,ikiwa ni sehemu ya mashtaka zaidi ya 100 yaliyowekwa dhidi yake.
Hii ni hukumu ndefu zaidi ya kifungo aliyopewa aliyekuwa mchezaji tenisi na kugeuka kuwa mwanasiasa ambaye amekuwa kizuizini tangu Agosti 2023.
Khan amekabiliwa na mashtaka kama vile kuvuja siri za serikali na kuuza zawadi za serikali- yote akikanusha akidai analengwa na mahasimu wake wa kisiasa.
Kesi hiyo mpya imetajwa na mamlaka za Pakistani kama kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo, ingawa Pakistani imewahi kushuhudia Sakata za kifedha awali zikihusisha viongozi wa zamani.
Khan na mkewe, Bushra Bibi, walituhumiwa kupokea ardhi kama rushwa kutoka kwa mfanyabiashara kupitia Al-Qadir Trust, na kutumia fedha za Uingereza kulipa faini za mfanyabiashara huyo.
Chama chake cha PTI kimesema kuwa ardhi hiyo ilikuwa kwa ajili ya kituo cha elimu ya kidini.
Licha ya kuwa jela, Khan bado anashikilia ushawishi mkubwa katika siasa za Pakistan, huku wafuasi wake wakifanya maandamano makubwa yaliyokithiri ukandamizaji wa polisi.