Takriban Wapalestina 10 wameuawa na karibu 40 kujeruhiwa na wanajeshi wa Israel wakati wa operesheni kubwa katika eneo la Jenin katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, wizara ya afya ya Palestina inasema.
Vyombo vya habari vya Palestina viliripoti kuwa siku ya Jumanne kulifanyika mashambulizi kadhaa ya anga huku idadi kubwa ya wanajeshi wakiingia katika mji huo na kambi yake ya wakimbizi, wakisaidiwa na ndege zisizo na rubani, helikopta na tingatinga za kivita.
Waziri Mkuu wa Israel alisema ilianzisha operesheni "kubwa na muhimu" ya "kushinda ugaidi" huko Jenin, ambayo kwa muda mrefu ilionekana kama ngome ya vikundi vya wapiganaji wa Palestina.
Hili linawadia siku tatu baada ya kuanza kwa usitishaji vita huko Gaza na kuongeza tishio la ghasia zaidi katika Ukingo wa Magharibi, ambapo washukiwa walowezi wa Israel pia walivamia Jumatatu usiku.
Wanajeshi wa kulinda usalama wa Palestina waliripotiwa kujiondoa kwenye baadhi ya maeneo walikokuwa karibu na kambi ya wakimbizi ya Jenin kabla ya vikosi vya Israel kuhamia.
Shirika rasmi la habari la Palestina, Wafa, baadaye lilinukuu vyanzo vya ndani vikisema kwamba vikosi vya Israeli "vilikuwa vinazingira kabisa" kambi ya Jenin, na kwamba tingatinga zenye silaha zilikuwa zimechimba mitaa kadhaa.
Mkurugenzi wa hospitali ya Serikali ya Jenin, Dk Wissam Bakr, pia aliambia shirika hilo kwamba madaktari watatu na wauguzi wawili ni miongoni mwa waliojeruhiwa kwa risasi za Israel.
Wizara ya afya ya Palestina iliripoti Jumanne jioni kwamba wanaume tisa na mvulana wa miaka 16, ambaye ilimtaja kama Mutaz Abu Tbeikh, waliuawa na vikosi vya Israeli huko Jenin.
Mwanaume mwingine alipigwa risasi na kuuawa na wanajeshi wa Israel katika kijiji cha Tianik, takriban kilomita 8 kaskazini-magharibi, iliongeza.
Vyanzo vya habari viliiambia BBC kuwa wengi wa waliouawa walikuwa raia.
Hata hivyo, jeshi la Israel na huduma ya usalama ya Shin Bet walisema Jumatano kwamba "wamewashambulia zaidi ya magaidi 10" wakati wa operesheni hiyo.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema katika taarifa kwamba operesheni ya Jenin - iliyoitwa "Iron Wall" - ilikuwa "hatua ya ziada katika kufikia lengo tuliloweka: kuimarisha usalama" katika Ukingo wa Magharibi.
Israel inaishutumu Iran kwa kusafirisha silaha na fedha kwa magendo kwa Hamas, Palestina Islamic Jihad na makundi mengine yenye silaha katika Ukingo wa Magharibi ili kuchochea machafuko.
Hamas na Palestina Islamic Jihad zote zilitoa wito kwa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuzidisha mashambulizi dhidi ya vikosi vya Israel ili kukabiliana na operesheni ya Jenin.