Wanajeshi 2 kutoka Tanzania wauawa DRC - Jeshi
HABARI
Published on 02/02/2025

Wanajeshi wawili kutoka Tanzania wameuawa nchini DRC kwa mujibu wa Jeshi la Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliotumwa kwa vyombo vya habari na Jeshi la Ulinzi la Tanzania , wanajeshi hao walifariki kutokana na mfululizo wa mashambulizi yaliofanywa na wapiganaji wa M23 katika maeneo ya Sake na Goma.

Taarifa hiyo imeongezea kuwa wanajeshi wengine wanne waliojeruhiwa wakati wa shambulio hilo wanapokea matibabu mjini Goma.

Taarifa hiyo ilisema: 'Kufuatia mashambulizi ya mfululizo katika maeneo ya Sake na Goma yaliofanywa na waasi wa M23 tarehe 24 na 28 Januari , jeshi la ulinzi la tanzania JWTZ limewapoteza askari wake idadi wa 2 na wengine idadi 4 kujeruhiwa. Majeruhi wanaendelea kupata matibabu mjini Goma'.

Taarifa hiyo iliotiwa saini na kaimu Mkurugenzi wa habari na uhusiano jeshi la ulinzi wa wananchi wa Tanzania kanali Gaudentius Gervas Ilonda imesemna kwamba taratibu za kusafirisha miili ya marehemu pamoja na majeruhi zinaendelea kupitia sekretariati ya SADC .

Aidha imeongezea kwamba ikundi vya wanajeshi wa Tanzania vilivyopo nchini DRC , vipo salama , Imara na vinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maelekezo ya uongozi wa SADC

Katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano wa dharura wa Jumuiya ya mataifa ya Afrika Kusini SADC siku ya Ijumaa Januari 31, mwenyekiti wa SADC Emmerson Mnangangwa ambaye pia ni Rais wa Zimbabwe, alisema kwamba hadi kufikia Januari 31 wanajeshi kutoka Malawi, Afrika Kusini na Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania walifariki katika makabiliano na kundi la M23.

Hadi sasa, Afrika Kusini imetangaza kuwapoteza wanajeshi 14 baada ya mmoja kuthibitishwa kufariki hospitalini usiku wa Jumamosi.

Na japo viongozi wa jumuiya hiyo wamesema kwamba kikosi cha SAMIDRC kilichoanza kazi baada ya kuondoka kwa kikosi cha jumuiya ya EAC cha EACRF , hakijatimiza majukumu yake ya kazi, kitengo cha usalama cha TROIKA kinachooongozwa na Tanzania katika SADC kinatarajiwa kufanya kikao cha dharura kutafuta mbinu za kuwaleta pamoja wahusika wote kwenye mzozo wa mashariki mwa DRC kuhakikisha kwamba vita vinasitishwa .

Aidha Troika imehitajika kuhakikisha kwamba njia ya kuingiza msaada wa kibinadamu zinafunguliwa kwa ajili ya kuwafaa waathiriwa wa machafuko yanayoendelea katika mji wa Goma na maeneo mengine.

Na japo kikosi cha SAMIDRC kimekabiliwa na majeraha na maafa ya wanajeshi kutoka mataifa husika, SADC imeeleza ahadi ya kuendelea kusimama na DRC kwa ajili ya kutafuta amani na kutetea utaifa wake na vile vile kuhakikishia usalama wake.

Jeshi la Ulinzi wa wananchi nchini Tanzania JWTZ limekuwa likishiriki shughuli za ulinzi wa amani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa na jumuiya za kikanda ikiwemo ni pamoja na nchini Lebanon, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati , Liberia Msumbiji pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

 

Comments
Comment sent successfully!