Mamlaka ya Sudan Kusini yatangaza amri ya kutotoka nje usiku kuanzia leo
HABARI
Published on 18/01/2025
Mamlaka ya Sudan Kusini yatangaza amri ya kutotoka nje usiku kuanzia leo
Maafisa wa usalama nchini Sudan Kusini wameweka amri ya kutotoka nje usiku baada ya maandamano kuzuka katika mji mkuu, Juba, Alhamisi.
Hii ni baada ya Waandamanaji kulenga biashara zinazomilikiwa na raia wa Sudan kufuatia ripoti za vitendo vya ukatili dhidi ya raia wa Sudan Kusini wakati majeshi ya serikali yalipodhibiti mji wa Wad Madani kutoka kwa Jeshi la RSF.
Mkuu wa Polisi wa Sudan ya Kusini jenerali Abraham Manyuat ametangaza (kupitia runinga ya taifa) kwamba amri ya kutotoka nje kuanzia jioni hadi asubuhi itaanza kutekelezwa usiku huu huko Juba na miji mingine.
‘’Ningependa kuwahakikisha raia kuwa polisi watalinda mali na maisha yenu.Wanajukumu kuhakikisha kuna utulivu na amani nchini humo.’’ anasema Jenerali Abraham Manyuat.
Naye Rais Salva Kiir ameomba utulivu na kuwasihi raia kuepuka mashambulizi ya kisasi.
Kwa mujibu wa gazeti la Xinhua balozi wa Sudan nchini Sudan Kusini amesema kamati ya uchunguzi imeundwa kuchunguza mauaji ya Wad Madani, yaliyotokea baada ya jeshi la Sudan Kusini kuchukua eneo hilo kutoka kwa waasi RSF.
"Kuna mataifa mengi yanayojihusisha na vita ndani ya Sudan. Kamati ya uchunguzi itafanya kazi kwa karibu na balozi wa Sudan Kusini aliyeko Port Sudan, na tutawapa taarifa raia wa Sudan Kusini na umma kuhusu hali ya raia wa Al Gezira," Anasema balozi huyo.
Sudan Kusini, ni nchi changa zaidi duniani, na ilipata uhuru kutoka kwa Sudan mwaka 2011.
Inakabiliwa na ukosefu wa utulivu wa muda mrefu, ghasia na umaskini uliokithiri, ambao hivi karibuni umechangiwa na baadhi ya mafuriko mabaya zaidi katika miongo kadhaa na wimbi kubwa la wakimbizi wanaokimbia vita nchini Sudan.
Comments
Comment sent successfully!