DR Congo inaituhumu Apple kwa kutumia madini yanayochimbwa katika maeneo ya mizozo
HABARI
Published on 18/12/2024

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imewasilisha malalamiko ya uhalifu nchini Ufaransa na Ubelgiji dhidi ya kampuni tanzu ya kampuni kubwa ya teknolojia ya Apple, ikiituhumu kutumia madini yanayochimbwa katika maeneo ya migogoro.

Wakifanya kazi kwa niaba ya serikali ya Congo, mawakili wamedai Apple inashiriki katika uhalifu unaofanywa na makundi yenye silaha ambayo yanadhibiti baadhi ya migodi mashariki mwa DR Congo.

Katika ukaguzi wake wa 2023 wa suala hilo, Apple ilisema inafuatilia chanzo cha madini hayo na kuboresha hatua za kufuatilia.

Mamlaka nchini Ufaransa na Ubelgiji sasa zitaangalia iwapo kuna ushahidi wa kutosha kuchukua hatua za kisheria.

Katika taarifa ya mawakili wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanadai kuwa madini ya bati, tantalum na tungsten huchukuliwa kutoka maeneo yenye migogoro na kisha "hutakatishwa kupitia minyororo ya kimataifa ya ugavi."

"Shughuli hizi zimechochea ghasia na migogoro kwa kufadhili wanamgambo na vikundi vya kigaidi na zimechangia ajira za kulazimishwa za watoto na uharibifu wa mazingira."

Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ni chanzo kikuu cha uchimbaji wa madini na hilo limechochea vita huko kwa miongo kadhaa.

Mashirika ya haki za binadamu kwa muda mrefu yamekuwa yakidai kuwa kiasi kikubwa cha madini kutoka kwenye migodi halali, pamoja na migodi inavyoendeshwa na makundi yenye silaha, husafirishwa hadi nchi jirani ya Rwanda na kuishia kwenye simu na kompyuta zetu.

 

Comments
Comment sent successfully!