Takriban watu 34 wamekufa kufuatia "dhoruba kali zaidi kuwahi kurekodiwa" kaskazini mwa Msumbiji, imesema Taasisi ya Kitaifa ya Kudhibiti Majanga (INGD).
Kimbunga Chido kilitua Msumbiji siku ya Jumapili, baada ya kusababisha uharibifu katika eneo la Bahari ya Hindi na kisiwa cha Mayotte.
Mamia wanahofiwa kufariki huko Mayotte - na watu kadhaa - ikiwa ni pamoja na zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea 200 wa Msalaba Mwekundu - wanadhaniwa kupotea.
INGD inaonya kuwa huenda idadi ya vifo ikaongezeka. Zaidi ya familia 34,000 za Msumbiji zimepoteza makazi yao, baada ya kimbunga cha upepo wa kasi ya karibu kilomita 260 kwa saa kupiga.
Shule, vituo vya afya na boti za uvuvi vimeharibiwa. Wengi wa waliouawa na Chido waligongwa na vitu vilivyokuwa vikianguka, kama vile kuta, amesema msemaji wa INGD Paulo Tomas.
Umeme na mawasiliano pia vimeathirika - kampuni ya umeme inayomilikiwa na serikali ya Electricidade de Moçambique (EDM) imetangaza kuwa karibu wateja 200,000 hawana nishati hiyo.
Mwaka jana Msumbiji ilipigwa na Kimbunga Freddy, mojawapo ya dhoruba zilizodumu kwa muda mrefu zaidi kuwahi kurekodiwa katika kizio cha Kusini cha dunia, kama si dunia nzima.
Shirika la Hali ya Hewa Duniani lilisema zaidi ya 180 nchini humo walikufa.