Wakati nilipoingia kwa mara ya kwanza katika mji wa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ilikuwa vigumu kwangu kusema kama nilikuwa nimeingia katika eneo linalokabiliwa na mzozo.
Wananchi wa Goma walikuwa wamejaa mitaani, kilomita chache kutoka mpaka wa Rwanda – abiria walikuwa wakielekea kazini, wajasiriamali walikuwa wakiuza bidhaa kando ya barabara, na madereva wa teksi walikuwa wakikimbizana kutafuta wateja.
Lakini ilichukua dakika chache tu kugundua kwamba kulikuwa na "serikali" mpya mjini.
Nilipofika katika kituo cha ukaguzi karibu na kituo cha polisi kilichokuwa kikiendeshwa na mamlaka za Congo, wapiganaji wenye silaha kutoka kwa kundi la waasi la M23 walisimamisha gari langu.
Wiki iliyopita M23 waliteka Goma, mji wa mashariki wenye watu karibu milioni mbili, baada ya shambulizi la haraka katika kanda ya mashariki ya Congo.
Angalau watu 700 katika mji huo waliuawa na karibu 3,000 kujeruhiwa wakati waasi walipokuwa wakipigana na jeshi la Congo na washirika wake, kulingana na Umoja wa Mataifa na serikali ya Congo.
M23, ambalo linajumuisha kabila la Watutsi, wanasema wanapigania haki za wachache, huku serikali ya Congo ikisema waasi hao wanaungwa mkono na Rwanda na wanatafuta kudhibiti utajiri mkubwa wa madini wa kanda ya mashariki.
Katika kituo cha ukaguzi, waasi wa M23 walitizama gari langu, walimuuliza dereva maswali machache, kisha walitwambia tuingie katika mji ulioharibiwa na mzozo ambao unaendelea.
Waasi hao hawakukutana na upinzani – ilikuwa kama vile walikuwa wamekuwepo kila wakati.
Nilielekea katika moja ya hospitali chache zinazotibu majeruhi na nilipoingia, kilio cha maumivu kilikukaribisha katika eneo hilo.
Nilikutana na Nathaniel Cirho, daktari ambaye, katika hali ya ajabu ya kubadilishana majukumu, aliketi kitandani katika hospitali akiwa na mkono wa kushoto uliofungwa kwa bendeji.
Bomu lililokuwa limeanguka liligonga nyumba iliyo karibu na yake na yeye na majirani zake waliguswa na marisau ya kombora.
"Nikapata majeraha mkononi mwangu. Mzee mwenye umri wa miaka 65 alijeruhiwa tumboni. Baada ya upasuaji, hakuamka tena alikata roho ," alisema kwa huzuni.
Wodi chache mbali, ajuza mmoja alikuwa amelala kitandani katika hospitali nyingine, akiwa ameunganishwa na tangi la oksijeni.
Alikuwa ameondoa risasi kutoka kwa mkono wake baada ya mapigano kuchacha katika eneo lake.
"Ghafla mkono wangu ulikufa ganzi, ndipo nilipotambua kwamba nilikuwa nimepigwa risasi," alisema, akijitahidi kuzungumza.
Kwa siku kadhaa, alikuwa akijitibu mwenyewe bila msaada. Aliniambia kwamba mwishowe alielekezwa kwa hospitali ya umma na waasi wa M23.
Mwanamke huyo aliomba kuhamishiwa katika hospitali ya kibinafsi, ambako sasa anapokea matibabu, kwa sababu hakuwa akipata huduma ya kutosha kutoka kwa madaktari walikuwa wamejaa sana.
Lakini hata katika hospitali hii ya pili, madaktari walikuwa wameshindwa kukabiliana na idadi inayoongezeka ya wagonjwa wanaokuja hospitalini.
"Tumetibu wengi wao kwa sababu tulikuwa na mipango ya dharura," alisema daktari mmoja, ambaye alikataa kutaja jina lake kwa sababu za kiusalama.
Aliongeza: "Jumapili wakati mapigano yalipoanza, tulipokea wagonjwa 315 na tukawatibu."
Lakini sasa, hospitali inahesabu wagonjwa zaidi ya 700, wakiwa na majeraha mbalimbali, daktari aliniambia.
Alizungumza kuhusu kupokea wagonjwa waliopigwa risasi "kichwani, wengine tumboni, mikononi na miguuni."
Wakati mashariki mwa Congo inakumbwa na misukosuko ya kisiasa, Ofisi ya Kamishina Mkuu wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imetahadharisha kuwa unyanyasaji wa kijinsia unatumika kama silaha ya vita na pande pinzani.
Daktari katika hospitali hii binafsi alithibitisha kauli ya Umoja wa Mataifa, akisema taasisi yake imepokea hadi sasa wahasiriwa 10 wa ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia.
Nje ya hospitali na kuelekea katikati ya mji, kulikuwa na mchanganyiko wa utulivu na uangalifu.
Watu walitembea karibu na magari manne yaliyokuwa yameharibiwa kwa risasi, wakishuhudia kile kilichotokea walipokuwa wakijihifadhi kwa usalama wakati wa mapigano.
Ingawa milio ya risasi na milipuko mjini Goma imepungua, sio maeneo yote ambayo shughuli za kila siku zimerejea kama kawaida.
Maduka machache yamefunguliwa katika baadhi ya mitaa, lakini sio kama vile awali. Benki kubwa pia zimefungwa.
Lakini watu wengi bado wana wasiwasi wakihofia uwezekano wa kurejea kwa mapigano katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
''Watu wanauoga...bado nina hofu kwasababu wale walioleta vurugu bado wako miongoni mwetu na hatujui kinachoendelea kwa sasa,'' mmiliki wa duka Sammy Matabishi anasema.
''Lakini cha kutamausha zaidi ni kuwa hakuna anayekuja kununua bidhaa madukani mwetu, wengi wamehamia Rwanda, (mji ulioko mpakani Congo) Bukavu, Kenya na Uganda''.
Anaongezea kuwa wafanyibiashara ambao huagiza bidhaa zao katika mataifa jirani wametatizika kusafirisha mizigo yao hadi mjini.
Wengi niliozungumza nao wanasema wameanza kuzoea kutawaliwa na kundi la M23.
Na kama mgeni katika nchi hiyo niliona juhudi za waasi za kuonyesha madaraka ya utawala wao.
Walikuwa wamedhibiti ofisi ya Gavana wa kijeshi wa Kivu Kaskazini, ambaye walimuua walipokuwa wakiingia na kuvamia mji wa Goma.
Wapiganaji walikuwa wakishika doria katika maeneo mbalimbali mjini, huku wengine wakizunguka mjini wakiwa wamebeba silaha.
Wakati nilikuwa Goma, sikuona afisa wa usalama yoyote wa jeshi la Congo.
Lakini, niliona magari ya maafisa wa polisi yaliyo na nembo za ''FARDC'', yakiwa ni maandishi ya kifaransa yanayotumika na wanajeshi wa Demokrasia ya Congo.
Karibu na kambi ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa (Monusco) – ambao wamedhamiria kulinda raia dhidi ya vikosi vya waasi – magwanda ya kijeshi, magazeti na risasi zilikuwa zimezagaa barabarani.
"M23 Walipofika hapa, walizunguka jeshi letu," alisema Richard Ali, ambaye anaishi karibu.
"Wengi walivua mavazi yao ya kijeshi, wakatupa silaha zao na kuvaa mavazi ya kiraia. Wengine walikimbia."
Wakati M23 wanasherehekea ushindi mkubwa, serikali ya Congo inaendelea kukataa madai kwamba waasi wa M23 wameiteka mji wa Goma kabisa.
Mamlaka inawashutumu M23 kwa kuchukua ardhi yao kinyume cha sheria – kwa msaada wa Rwanda – na inaahidi kurejesha maeneo yaliyopotea.
Ingawa Rwanda ilikuwa ikikanusha mara kwa mara kuhusika na kupiga jeki waasi wa M23, majibu yake yameanza kugeuka na kuwa ya kujitetea, msemaji wa serikali akidokeza kuwa vita vinavyoshuhudiwa kariu na mpaka wao ni tishio kwa usalama wao.
Waasi sasa wanadaiwa kusogea kusini kuelekea Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, na wameapa kufika katika mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa.
Kwa sasa, Goma ndio mji wanajivunia kuuteka.
Hali ilivyo sasa katika mji huo unachora taswira vile hali itakavyokuwa iwapo M23 wataendelea kuteka na kudhibiti miji mingine zaidi.