Rais John Dramani Mahama, ameapishwa kushika wadhifa huo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Black Star Square katika mji mkuu wa Ghana, Accra.
Ni kufuatia ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwezi uliopita. Na kwa mara ya kwanza, nchi hiyo pia ina Makamu wa Rais mwanamke, Profesa Jane Naana Opoku Agyemang.
Mapema leo, Wabunge na spika wapya waliapishwa. Mahama amewahi kuwa Rais wa Ghana kuanzia 2012 hadi 2017.
Viongozi 21 wa nchi akiwemo Rais wa Nigeria na Mwenyekiti wa ECOWAS Bola Tinubu walikuwepo kushuhudia tukio hilo.
Mahama anachukua wadhifa huo wakati ambapo Ghana inapata nafuu kutokana na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi kuwahi kutokea. Matarajio ni makubwa, na Mahama ameahidi kuletea mageuzi ya uchumi.