Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema anayemaliza muda wake baada ya kushindwa katika uchaguzi na Tundu Lissu amesema mchakato wa uchaguzi huo umekiacha chama hicho na majeraha.
Mbowe amesema japo uchaguzi umefanyika katika misingi ya uhuru, haki na uwazi kama ambavyo aliahidi awali lakini amesema mchakato wa kampeni umeacha majeraha na amemtaka Lissu na viongozi wengine waliochaguliwa kuleta maridhiano ndani ya chama.
“Mimi niliahidi kuwa kama ningeshinda ningeliunda kamati ya ukweli na maridhiano ili watu wazungumze na kutibu majeraha yaliyoletwa na kampeni … sasa kama mnaniheshimu kama baba, basi nawaagiza Lissu na viongozi wenzako wapya mlete maridhiano baada ya majeraha yaliyoletwa na kampeni,” amesema.
Mbowe pia amewataka viongozi wapya kusimama na katiba ya chama hicho na kujizui kuwa na kiburi.
Kuhusu mustakabali wake kisiasa, Mbowe amesema anachukua likizo na ataendelea kujikita katika kufanya biashara zake na kuendelea kukishauri chama.
“Nimepewa likizo ya lazima, na nitaenda kwenye biashara zangu nitafute pesa ana nitaendelea kutoa ushauri kwa chama…Nashukuru nimepewa likizo hii kidemokrasia na katika mfumo ambao nimeujenga mwenyewe… kuna watu waliniambia nijitoe kwenye uchaguzi nitaadhirika, nikawaambia nitafia demokrasia.”