Nyota wa Bollywood hayuko tena hatarini baada ya kudungwa kisu
BURUDANI
Published on 18/01/2025
Seif Ali Khan: Nyota wa Bollywood hayuko tena hatarini baada ya
kudungwa kisu
Muigizaji maarufu wa Bollywood Saif Ali Khan amefanyiwa upasuaji na hayuko tena hatarini baada ya kudungwa kisu na mvamizi nyumbani kwake, timu yake imesema.
Shambulio hilo lilitokea mapema Alhamisi asubuhi katika mji wa Mumbai nchini India, ambapo Khan anaishi na familia yake.
Polisi wa jiji waliambia BBC Marathi kwamba mwigizaji huyo alijeruhiwa baada ya ugomvi kuzuka kati yake na mtu asiyejulikana ambaye aliingia nyumbani kwake muda wa saa sita usiku.
Polisi wameunda timu kuchunguza tukio hilo.
"Khan amefanyiwa upasuaji na hayuko tena hatarini. Kwa sasa anaendelea kupata ahueni na madaktari wanafuatilia hali yake," timu ya Khan ilisema katika taarifa.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya upasuaji huo, Dk Nitin Dange wa Hospitali ya Lilavati, ambako Khan amelazwa, alisema kuwa mwigizaji huyo “alipata jeraha kubwa kwenye uti wa mgongo upande wa juu kutokana na kisu alichodungwa”.
"Upasuaji ulifanyika ili kutoa kisu kilichokwama na kurekebisha maji ya uti wa mgongo yaliyovuja. Majeraha mengine mawili ya kina kwenye mkono wake wa kushoto na jingine shingoni yalirekebishwa na timu ya upasuaji wa kubadili maumbile," alisema.