Ronaldo kugombea urais wa shirikisho la soka Brazil
MICHEZO
Published on 18/12/2024

Gwiji wa Brazil, Ronaldo Luís Nazário de Limaametangaza atawania kiti cha urais katika chama cha soka cha nchi hiyo na anataka "kurudisha heshima" ya timu ya taifa.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 48, atagombea kuchukua nafasi ya rais wa sasa wa Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) Ednaldo Rodrigues.

Brazil, ambayo ina rekodi ya kushinda mara tano Kombe la Dunia, ilishinda kombe hilo mara ya mwisho mwaka 2002 na haijasonga mbele zaidi ya hatua ya robo fainali tangu wakati huo.

"Miongoni mwa mamia ya mambo yanayonipa motisha kuwa mgombea wa urais wa CBF ni kurejesha heshima ambayo timu ya taifa imekuwa nayo siku zote na hakuna mtu mwingine aliye nayo leo," amesema.

Muhula wa Rodrigues utaendelea hadi Machi 2026 na uchaguzi wa urais lazima ufanyike katika miezi 12 kabla ya wakati huo.

Ronaldo, mshindi wa Kombe la Dunia mwaka 1994 na 2002, anashika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa kombe la dunia nyuma ya Miroslav Klose wa Ujerumani aliyefunga mabao 15 katika mechi 19 alizocheza.

Maisha ya soka ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Real Madrid yalidumu kwa miaka 17 na kujumuisha mataji mawili ya Copa America na medali ya shaba ya Olimpiki.

Brazil wameshinda Copa America mara moja tangu Ronaldo alipostaafu kimataifa mwaka 2011 na kutolewa nje ya Kombe la Dunia la 2022 na Croatia katika robo fainali.

 

Comments
Comment sent successfully!