Maafisa wa Urusi wamezishutumu nchi za Magharibi kwa kupanga mauaji ya Luteni Jenerali Igor Kirillov, wakisema ni kutokana na jukumu lake la "kufichua uhalifu wa Waanglo-Saxon."
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Jimbo la Duma, Andrei Kartapolov, ameapa kuwatafuta na kuwaadhibu "wale waliohusika kuandaa na kutekeleza" mauaji ya Kirillov "bila kujali ni nani au wako wapi."
Kwenye Telegram, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova ameandika, Kirillov "alitumia miaka mingi kufichua uhalifu wa Waanglo-Saxons."
Jenerali mstaafu wa jeshi Andrei Gurulyov anasema, Kirillov ni mtu "aliyeelewa na kufuatilia shughuli zote za uhalifu za Marekani na satelaiti zake, ikiwa ni pamoja na maabara zao za uhalifu na silaha za kemikali na za kibaiolojia."
Uingereza ilimtaja Kirillov mwezi Oktoba, ikimwita "msemaji muhimu wa habari za Kremlin, akieneza uwongo ili kuficha tabia hatari za Urusi."
Kamati ya uchunguzi ya Urusi imeelezea mauaji ya Luteni Jenerali Kirillov kuwa ni "kitendo cha kigaidi."
Msemaji Svetlana Petrenko anasema: "Tukio hilo limeainishwa kama kitendo cha kigaidi, mauaji, usafirishaji haramu wa silaha."