Israel imesema kuwa moja ya mashambulizi yake ya angani nje ya mji wa Beirut yalimuua Hashem Safieddine, aliyetazamiwa kuwa mrithi wa kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah.Taarifa hiyo imesema Safieddine aliuawa wiki tatu zilizopita kufuatia shambulio katika vitongoji vya kusini mwa Beirut. Hakujawa na kauli ya haraka kutoka kwa Hezbollah inayothibitisha hatima ya Safieddine, ambaye alikuwa mhubiri mwenye ushawishi mkubwa. Israel imesema shambulizi hilo pia liliwauwa viongozi wengine 25 wa Hezbollah. Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani aliyeko nchini Israel Antony Blinken amewataka viongozi kukitumia kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar kama fursa ya kumaliza vita Gaza na kufanikisha mpango wa kuwachiwa huru mateka. zaidi anasema "Tangu Oktoba 7, mwaka mmoja uliopita, Israel imefanikisha malengo yake ya kimkakati linapokuja suala la Gaza. Kuhakikisha kilichotokea Oktoba 7 hakirudiwi kamwe. Sasa kuna mambo mawili yaliyobaki: kuwarejesha nyumbani mateka na kumaliza vita kwa kuelewa kitakachofuata." Nchini Lebanon, jeshi la Israel leo limetoa wito mpya wa kuhamishwa wakaazi wa mji wa kusini mwa Lebanon wa Tyre, likionya kuhusu operesheni zinazokaribia kuanza zikililenga kundi la Hezbollah