Jeshi la Israel latangaza kumuua kiongozi wa Hezbollah
HABARI
Published on 04/11/2024

Jeshi la Israel lilitangaza Jumatatu kuwa limemuua "kamanda mkuu wa Hezbollah" ambaye lilisema alikuwa akisimamia urushaji wa makombora ya vifaru dhidi ya wanajeshi wa Israel kusini mwa Lebanon.

Jeshi lilisema kuwa kiongozi wa Hezbollah katika eneo la Barashi kusini mwa Lebanon, Abu Ali Reda, "aliuawa" katika shambulio la anga bila kutaja tarehe.

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, Abu Ali Reda "alikuwa na jukumu la kupanga na kutekeleza mashambulizi ya roketi na kurusha makombora ya vifaru kwa vikosi vya IDF, na pia alisimamia shughuli za wapiganaji wa Hezbollah katika eneo hilo."

Hezbollah bado haijatoa taarifa yoyote ya kukanusha au kuthibitisha habari za kifo cha Abu Ali Reda.

Hivi karibuni Israel imewaua viongozi wengi waandamizi wa Hezbollah, hasa Katibu Mkuu wa chama hicho Hassan Nasrallah mnamo Septemba 27 katika shambulio kali katika viunga vya kusini mwa Beirut.

Kwa upande wake, Hezbollah ilitangaza Jumatatu asubuhi kwamba imeulenga mji wa Safed na kaskazini mwa Haifa kwa masafa makubwa ya makombora "kuwaunga mkono wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na kuunga mkono upinzani wao, na katika kuilinda Lebanon na nchi yake."

 

Comments
Comment sent successfully!