Jeshi la Israel linasema kuwa lilimuua kiongozi wa kidini aliyekuwa anadokezwa kumrithi aliyekuwa kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, katika shambulio la anga karibu wiki tatu zilizopita.
Hashem Safieddine alifariki katika mashambulizi ya anga kwenye viunga vya kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut, kulingana na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF).
Hezbollah, shirika lenye nguvu la Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Lebanon linalopigana na Israel, halijathibitisha kifo cha Safieddine.
Kiongozi wake wa awali, Nasrallah, aliuawa na mashambulizi ya anga ya Israel huko Beirut tarehe 27 Septemba.
Baada ya mashambulio ya anga karibu na uwanja wa ndege wa mji huo tarehe 4 Oktoba, maafisa wa Hezbollah walisema wamepoteza mawasiliano na Safieddine, huku vyombo vya habari vya Marekani vikiwataja maafisa wa Israel wakisema mhubiri huyo ndiye aliyekuwa mlengwa wa shambulio hilo.
Milipuko mikubwa ilitikisa jiji usiku huo, ikiacha moshi mwingi ambao ungeweza kuonekana hadi asubuhi.