Guterres alaani shambulizi la Iran baada Israel kumpiga marufuku
HABARI
Published on 03/10/2024

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel, baada ya kupigwa marufuku na nchi hiyo.

Akizungumza na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, António Guterres alisema ni wakati mwafaka kusitisha kile alichokiita "mzunguko mbaya wa ghasia za nipe nikupe" katika Mashariki ya Kati.

Hapo awali Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Israel Katz alitangaza kuwa Guterres hana ruhusa ya kuingia nchi hiyo kwa kuwa "katibu mkuu anayepinga Israel na anaunga mkono magaidi".

Maoni hayo yalitolewa kujibu Guterres akitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, lakini bila kutaja haswa shambulio la Iran.

Wakati huo huo Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amelitaja shambulizi la makombora la Iran dhidi ya Israel kuwa ni ongezeko kubwa la mivutano katika eneo la Mashariki ya Kati.

Linda Thomas-Greenfield anasema baraza la usalama la umoja huo linapaswa kuchukua hatua "haraka".

Comments
Comment sent successfully!