Nje ya Mahakama hiyo wakili anayetetea watuhumiwa , Godfrey Wasonga amesema hawakuridhishwa na hukumu hiyo kwani kuna baadhi ya vifungu vimekiukwa.
Uamuzi huo ulitolewa katika Kesi ya Jinai namba 23476 ya mwaka 2024, ambapo watu waliohukumiwa walitambuliwa kuwa MT 140105 Clinton Damas, anayejulikana pia kama "Nyundo," askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ); C.1693 Askari Magereza Praygod Mushi; Nickson Jackson, anayejulikana pia kama "Machuche"; na Amin Lema, anayejulikana kwa jina la "Kindamba."
Kisa cha binti huyo kilisababisha Kamanda wa polisi katika mji mkuu wa Tanzania, Dodoma, kuondolewa kwenye wadhifa wake kufuatia matamshi ya kutatanisha ambapo alimhusisha mwathiriwa anayedaiwa kubakwa na genge na biashara ya ngono.
Mapema mwezi Agosti, video iliyokuwa ikionyesha msichana akishambuliwa ilisambaa, na kusababisha kilio katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
Baadaye jeshi la polisi nchini humo lililazimika kuomba radhi kuhusu matamshi ya kamanda huyo na kuahidi uchunguzi wa kina .
"Jeshi la polisi linapenda kuomba radhi kwa kila mtu ambaye aliguswa na kukerwa na taarifa hiyo inayosambazwa kwenye vyombo vya habari wakati ufuatiliaji ukifanyika ili kupata usahihi wake," msemaji wa polisi wa taifa David Misime alisema wakati huo .
Bw Msime aliongeza kuwa katika maoni yake kwa gazeti la ndani la Mwananchi, Kamanda wa Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya alisema hata kama mwanamke huyo alikuwa mfanyabiashara ya ngono, "hakustahili kutendewa hivyo".
Maneno hayo hata hivyo hayakuonekana kwenye ripoti ya Mwananchi- BBC iliwasiliana na gazeti hilo kwa ufafanuzi.
Akijibu ripoti ya Mwananchi, wakili Peter Madeleka alisema kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba maoni ya Bi Mallya yalikuwa ni "ushahidi wa ukatili wa polisi kwa haki za wanawake".
Fatma Karume, mwanasheria na mwanaharakati maarufu, naye alionyesha kukerwa na kuandika kwenye X: "Wanaojiuza hawawezi kubakwa katika nchi hii?"
Katika video hiyo iliyoonekana kumuonyesha mwanamke huyo akibakwa, inasemekana washukiwa walimhoji, hivyo kumlazimu kuomba msamaha kwa mtu aliyejulikana kwa jina la “afande”.
Nchini Tanzania neno "afande" mara nyingi linatumika kumaanisha askari au polisi, hivyo wanaharakati wengi na watumiaji wa mitandao ya kijamii walionyesha kukerwa na tukio la unyanyasaji wa kijinsia kutekelezwa kwa amri ya askari mmoja wa vyombo vya usalama.
"Uchunguzi ulibaini kuwa vijana hao hawakuwa wakifuata maagizo kutoka kwa maafisa wowote; walikuwa wamekunywa pombe na dawa za kulevya," Bi Mallya aliambia Mwananchi wakati huo.
"Hata hivyo mwanamke husika alionekana kujishughulisha na biashara ya ngono," alisema.
Kufuatia kero za wananchi kuhusu maoni ya Bi Mallya, polisi wa taifa la Tanzania walisema amehamishwa hadi makao makuu ya polisi, ingawa haijabainika iwapo hii ilikuwa ya muda au ya kudumu.
Pia haijafahamika ni lini video hiyo ya mtandaoni ilirekodiwa lakini mwathiriwa huyo aliripotiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, kitongoji cha jiji kubwa zaidi nchini, Dar es Salaam.
Washukiwa wanne walifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa ubakaji wa genge na kujihusisha na vitendo visivyo vya asili.