Putin apendekeza sheria mpya kuhusu matumizi ya silaha za nyuklia
HABARI
Published on 26/09/2024

Vladimir Putin anasema Urusi itachukulia shambulio kutoka kwa taifa lisilo la nyuklia ambalo liliungwa mkono na lenye silaha za nyuklia kuwa "shambulio la pamoja", katika kile kinachoweza kuzingatiwa kuwa tishio la kutumia silaha za nyuklia katika vita vya Ukraine.

Katika hotuba yake muhimu Jumatano usiku, rais wa Urusi alisema serikali yake inazingatia kubadilisha sheria na masharti ambayo Urusi itatumia zana zake za nyuklia.

Ukraine ni taifa lisilo la nyuklia ambalo hupokea msaada wa kijeshi kutoka kwa Marekani na nchi nyingine zenye silaha za nyuklia.

Maoni yake yanakuja wakati Kyiv inatafuta idhini ya kutumia makombora ya masafa marefu ya Magharibi dhidi ya maeneo ya kijeshi nchini Urusi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesafiri kwenda Marekani wiki hii na anatazamiwa kukutana na Rais wa Marekani Joe Biden mjini Washington siku ya Alhamisi, ambapo ombi la Kyiv linatarajiwa kuwa ajenda kuu.

Ukraine imeingia katika ardhi ya Urusi mwaka huu na inataka kulenga ngome ndani ya Urusi ambayo inasema inatuma makombora nchini Ukraine.

Akijibu matamshi ya Putin, mkuu wa wafanyakazi wa Zelensky Andriy Yermak alisema Urusi "haina kitu kingine chochote zaidi ya ulaghai wa nyuklia wa kutisha ulimwengu".

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alielezea maoni hayo kama "ya kutowajibika kabisa" katika mahojiano ya televisheni ya MSNBC.

Mshirika wa Urusi, China pia imetoa wito wa utulivu, huku ripoti kuwa Rais Xi Jinping amemuonya Putin dhidi ya kutumia silaha za nyuklia

Comments
Comment sent successfully!