Neema yawazukia Wafungwa huko Nigeria baada ya jela kusombwa na mafuriko
HABARI
Published on 17/09/2024

Mamlaka za Nigeria zinasema kuwa zaidi ya wafungwa 270 hawajulikani waliko baada ya kutoroka rumande wakati mafuriko makubwa yalipoharibu gereza moja katika moja mjini Maiduguri kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo.

Kufikia sasa, saba kati yao wamerudi kizuizini.

Mafuriko hayo yalisababishwa na kuporomoka kwa bwawa kufuatia mvua kubwa iliyonyesha.

Takriban watu 30 wamefariki kutokana na mafuriko hayo na mamia ya wengine wamelazimika kuyahama makazi yao huko Maiduguri- mji mkuu wa jimbo la Borno.

Gavana wa jimbo la Borno Babagana Zulum alielezea uharibifu huo kuwa ''mbaya sana.''

Hii ni mara ya kwanza kwa mamlaka ya Nigeria kutangaza hadharani idadi ya wafungwa waliotoroka kizuizini.

Idara ya Magereza ya Nigeria (NCoS) ilisema Jumapili kwamba baada ya kuta za gereza la ulinzi kuharibiwa, wafungwa walikuwa katika harakati za kuhamishwa na baadhi walifanikiwa kutoroka wakati wa "shughuli ya kuwamisha".

Gavana Zulum hapo awali aliambia BBC kwamba baadhi ya waliotoroka ni wanamgambo wa kundi la la Boko Haram.

Lakini haijabainika ni wangapi kati ya wafungwa hao waliotoroka wanahusishwa na kundi hilo kijihadi.

Comments
Comment sent successfully!