Zaidi ya wafungwa wanawake 260 walishambuliwa kingono wakati wa jaribio kutoroka gereza kuu la Makala nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mwezi huu, ripoti ya ndani ya Umoja wa Mataifa iliyoonekana na shirika la habari la Reuters ilieleza.
Takriban watu 129 waliuawa wakati walinzi wa gereza walipotumia silaha za moto dhidi ya wafungwa wanaojaribu kutoroka gerezani mjini Kinshasa ambapo takwimu rasmi zinasema lina uwezo wa kuhifadhi wafungwa 1,500 lakini lina wafungwa zaidi ya 15,000.
Serikali ilisema baada ya jaribio hilo kutokea nyakati za alfajiri hapo Septemba 2, wanawake walishambuliwa kingono bila ya kutaja idadi kamili. Lakini ripoti ya ndani ya Umoja wa Mataifa iliyoonekana na Reuters kuhusu tukio hilo, ilisema wanawake 268 kati ya 348 waliofungwa katika jela ya Makala wamefanyiwa manyanyaso ya ngono, ikiwemo ubakaji wakati vurugu zilipotokea.
Miongoni mwao wasichana 17 walikuwa chini ya umri wa miaka 19.