Mwanaume mwenye silaha ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi wa Ujerumani karibu na kituo cha Nazi na ubalozi mdogo wa Israel katika mji wa kusini wa Munich.
Mwanamume huyo, aliyetambuliwa na polisi kama raia wa Austria mwenye umri wa miaka 18, aliuawa wakati wa kurushiana risasi na maafisa.
Polisi walisema mwanamume mmoja alikuwa ameonekana katika eneo hilo akiwa amebeba bunduki ndefu.
Ubalozi mdogo wa Israel ulikuwa umefungwa wakati huo kwa ajili ya ibada ya kumbukumbu ya miaka 52 ya shambulio la wanamgambo wa Kipalestina katika Michezo ya Olimpiki ya Munich mwaka 1972, ambapo wanariadha 11 wa Israel na afisa wa polisi waliuawa.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Bavaria Joachim Herrmann alisema nia ya tukio hilo haikubanishwa mara moja lakini huenda lilihusishwa na maadhimisho hayo.
Aliongeza kuwa "inawezekana" mtu mwenye silaha alikuwa amepanga kushambulia "taasisi ya Israeli".
Polisi walisema hakukuwa na dalili zozote za washukiwa wengine katika tukio hilo la Alhamisi.
Mkuu wa polisi wa Munich Thomas Hampel alisema mtu huyo alikuwa amejihami kwa bunduki ya zamani ya kuwinda.
Vyombo vya habari vya Ujerumani viliripoti kwamba awali alikuwa anajulikana na vyombo vya usalama kwa tuhuma za kuunga mkono makundi ya Kiislamu yenye vurugu, lakini polisi walikataa kuzungumzia ripoti hizo.
Helikopta ya polisi ilizunguka eneo hilo na umma kutakiwa kutoweka picha za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii.
Ni taarifa yake mwandishi wetu Elikana Felix @elikana_officialtz