Mahakama moja nchini Rwanda inayoshughulikia kesi za uhalifu wa mauaji ya kimbari imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela mkurugenzi wa zamani wa taasisi ya kilimo Venant Rutunga kwa kumkuta na hatia ya kuwa mshirika katika mauaji dhidi ya watutsi mwaka 1994.
Rutunga alirejeshwa nchini Rwanda mwaka 2021 na mamlaka ya Uholanzi ili kujibu mashitaka ya mauaji ya kimbari ambayo anakanusha.
Mahakama imesema kwamba wakati wa mauaji ya kimbari aliomba msaada wa wanajeshi waliotumwa kushika doria kwenye ofisi za taasisi hiyo na baadae wakafanya mauaji ya watutsi zaidi ya elfu 1 waliokuwa wamejificha eneo hilo na mengine jirani.
Awali Katika vikao vya kesihiyo Venant Rutunga alisema yeye alileta wanajeshi hao kwa nia njema ya kulinda taasisi hiyo na kwamba kamwe hawezi kuwajibishwa kutokana na mauaji yaliyotekelezwa na wanajeshi hao.
Leo mahakama imesema Daktari Rutunga hakumuua mtu yeyote kwa kutumia silaha lakini jukumu lake kubwa ni kuwaleta wanajeshi hao licha ya kufahamu kuwa wanakuja kutekeleza mauaji ya kimbari.
Mahakama imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela.
Jaji amesema angepewa kifungo cha maisha jela lakini kwamba mahakama imeamua kumpunguzia hukumu kutokana na mwenendo wake wakati wa kesi.
Ana siku 30 za kukata rufaa na wakili wake Sebaziga Sophonie ameiambia BBC ‘’tuna siku 30 za kutafakari uwezekano na njia za kukata rufaa’’ Ni Taarifa yake Mwandishi wetu Elikana Felix @elikana_officialtz