Miaka 24 ya Mkutano wa Afrika na China, Afrika itarajie kuambulia nini?
HABARI
Published on 05/09/2024

 

j

Chanzo cha picha,Wizara ya mambo ya nje ya China

Maelezo ya picha,Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa China Xi Jiping, katika Mkutano wa China na Afrika wa mwaka 2024
  • Author,

Leo (Alhamis) Rais wa China Xi Jinping atafungua mkutano wa tisa kati ya China na Afrika huko Beijing. Ukijulikana kama Forum on China–Africa Cooperation (FOCAC), mkutano huu ulianzishwa mwaka 2020 hufanyika kila baada ya miaka mitatu.

Katika hotuba yake, Xi anatarajiwa kupigia chepuo sera na mkakati mpya wa China wa bidhaa za kijani kama vile magari ya umeme na vifaa vingine vinavyotumia nishati ya jua.

Takribani viongozi 50 wa Afrika wamefika Beijing kuhudhuria mkutano ambao wengi wao huusubiria kwa hamu. Hata wale ambao huwa wavivu kuzuru maeneo mengi ya ndani ya nchi zao, huhakikisha hawaukosi mkutano huu.

Tofauti na wanapohudhuria mikutano katika nchi kama Marekani vile, wakiwa China, viongozi wa Afrika hupokelewa kwa mtindo na mbwembwe za hali ya juu. Kutandikiwa mazulia mekundu na fursa ya kukutana ana kwa ana na rais wa nchi hiyo, huwafanya wajisikie ufahari na kuwa na hadhi sawa na mwenyeji wao

Fursa ya kupata msaada wa kifedha na makubaliano ya kibiashara na uwekezaji ni vichocheo vingine vinavyowavutia kuhudhuria mkutano huu

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, kwa mfano, anatarajia kutafuta fedha za miradi ya mawasiliano vijijini, ujenzi wa njia za kusafirisha umeme, ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi (VETA) na barabara za visiwani Zanzibar

Rais wa Kenya William Ruto yeye pamoja na mambo mengine anatafuta fedha za miradi ya miundombinu ikiwa ni Pamoja na kukamilisha Reli ya Standard Gauge (SGR) inayounganisha pwani ya Kenya na Uganda na mfumo wa usafiri unaotumia teknolojia kwa ajili ya mji mkuu, Nairobi

Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini anatilia mkazo mkakati wa makusudi utakaosaidia nchi yake kuweza kupeleka bidhaa zao nyingi pia nchini China, badala ya China tu kuwa na uwezo mkubwa wa kuleta bidhaa zao Afrika

Kwa nchi zilizojaaliwa madini muhimu na adimu kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zimbabwe, na Zambia, wanatarajiwa kuzungumzia zaidi haja ya China katika kuwasaidia kujenga uwezo wa kuongeza thamani katika madini yao kama vile lithium na cobalt.

China, kwa upande mwingine, vipaumbele vyao si vingi sana na viko wazi. Pamoja na kuendeleza ushawishi wa fursa za biashara na uwekezaji Afrika, hivi sasa wameanza kuweka msisitizo mkubwa wa kuhamishia uwekezaji na bidhaa za kijani – hasa solar na magari ya umeme.

Msukumo huu unakuja baada ya China kuachana na kishindo chake cha miradi mikubwa kama reli, barabara na madaraja, na kuchukua uelekeo mpya ambao Rais Xi ameutambulisha kama “miradi midogo na maridadi” (small and beautiful projects)

Lakini haraka ya China kuligeukia soko la Afrika kwa bidhaa hizi za kijani linatokana pia na kubanwa na nchi kama Marekani ambayo imekuwa ikiiwekea China vikwazo vingi vya kibiashara, alimladi tu kuikatisha tamaa na kuidhibiti isiliteke soko la marekani wakati ambapo Marekani inawalinda wazalishaji wake wa ndani.

f

Chanzo cha picha,@WilliamsRito

Maelezo ya picha,Ujumbe wa Kenya katika mkutano wa China na Afrika katika mazungumzo na Rais Xi Jimping

Kwa mujibu wa takwimu za China-Africa Trade Index, zilizochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2023, hadi kufikia mwaka jana uuzwaji wa magari ya umemme ya China barani Afrika ulikuwa umeongezeka kwa asilimia 291

Hili ni eneo ambalo nchi kama Ethiopia inaliangalia sana kwasasa. Katika mpango wake wa miaka 10 (2021-2030), nchi hiyo ina mpango wa kuingiza mabasi ya umeme 5000 na magari ya kawaida zaidi ya 100,000. Mwaka jana Ethiopia ilipiga marufuku uingizwaji wa magari yasiyo ya umeme nchini humo na kupunguza kwa kiasi kikubwa kodi ya uingizwaji wa magari ya umeme.

Ethiopia ndio nchi barani Afrika iliyofanikiwa sana kutengeneza maeneo maalum ya viwanda na biashara (Special Economic Zone) kama za China ambazo zimefanikiwa sana kuimarisha viwanda vya nguo. Akiwa Beijing wiki hii, Waziri Mkuu Abiy Ahmed anatarajiwa kuweka msisitizo katika kuimarisha viwanda vya utengenezwaji wa magari ya umeme na bidhaa zingine za kijani.Ni ngumu kujua kwa hakika viongozi wa Afrika wataambulia nini hasa kutoka katika mkutano huu. Hata hivyo wachambuzi wengi wanaamini hapatakuwa na mipango mikubwa yenye ahadi ya pesa nyingi kama zamani

“(Sana sana) tutaona mikataba midogo midogo tu mingi, si zaidi ya dola milioni 50, mingi ikilenga nishati ya kijani na mawasiliano ya simu ambayo bila shaka itasaidia lakini haitabadilisha kwa kiasi kikubwa mwelekeo wa sasa (wa kibiashara na uwekezaji kati ya China na Afrika)” anaandika Eric Olander, Mhariri Mkuu, China-Global South Project

Kwa sehemu – pamoja na kubadilisha uelekeo na vipaumbele – China imepunguza sana kiwango cha fedha inachopeleka Afrika. Ni mwaka jana tu ndio China iliongeza kidogo kiwango cha mikopo kwa Afrika kufikia dola bilioni 4.61 tangu mwaka 2016 ambapo ilitoa mikopo kwa Afrika yenye thamani ya takribani dola bilioni 28.4.

Lakini China imekuwa ikikosolewa sana pia kwa usiri mkubwa wa taarifa za kina kuhusu miradi ya makubaliano na kukosekana na nyenzo za kufuatilia na kupima maendeleo ya ahadi zinazotolewa katika mikutano hii

Wachambuzi wengi wanaonya kwamba usiri huu unaondoa shauku ya vitu mahsusi vya kufuatilia katika mkutano huo kiasi kwamba mijadala mingi huishia katika kuhisi tu kitakachojili huku makisio mengi yakijirudia kutoka mkutano mmoja hadi mwingine

wa serikali yake.

Getty Images

Chanzo cha picha,Getty Images

Nyumbani barani Afrika, wengi wanakosoa msululu wa mikutano ya aina hii, ambapo viongozi wa bara zima la Afrika wanaitwa nje ya nchi kukutana na kiongozi mmoja wa nchi wenyeji.

Mbali na FOCAC kuna takribani mikutano mingine 10 ya nchi kubwa kama Marekani na zingine ndogo kama Italy zinazowakusanya viongozi wa Afrika nyumbani kwao katika mikutano iliyopewa jina la Africa+1

“Mtu anaweza kusema kwamba Afrika inaweza kukosa fursa za kiuchumi na maendeleo ikiwa itakwepa mikutano hii. Lakini badala ya kushiriki kwenye mikutano ya 1+ Afrika au kuiepuka kabisa, nchi za Afrika zinapaswa kutumia majukwaa yaliyopo kama Umoja wa Afrika au mashirika ya kieneo kama Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) au Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuandaa nchi zinazotaka kufanya mikutano na mataifa ya Afrika. Jumuiya ya Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia (ASEAN) mara kwa mara huandaa mikutano ya ASEAN + 3 na ASEAN + 6 ambayo inaweza kutoa maarifa muhimu” ameandika Abubakar Abubakar Usman, mhadhiri Universiti Malaya.

Wakati akiwa ndio kaingia tu madarakani, Ruto aliwaambia wahudhuriaji katika warsha iliyoandaliwa na Mo Ibrahim Foundation kwamba yeye na baadhi ya viongozi wa Afrika wameapa kutokuhudhuria mikutano kama hii ya FOCAC

"Sisi (viongozi fulani wa Afrika) tumeamua kwamba si busara kwenda kukaa mbele ya mheshimiwa mmoja kutoka sehemu nyingine... na wakati mwingine tunatendewa vibaya. Tunapakiwa kwenye mabasi kama watoto wa shule."

Hata hivyo Ruto tayari amewasili Beijing akiambatana na mke wake, Waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Raila Odinga na viongozi wengine waandamizi

Comments
Comment sent successfully!