Zaidi ya wanajeshi elfu moja wa Uingereza wapo tayari kwa operesheni ya kuwaondoa raia wa Uingereza watakaohitaji kuhamishwa kutoka Lebanon.
Maandalizi yanafanywa kujibu onyo la Ofisi ya Mambo ya Nje kwamba hali katika Mashariki ya Kati inaweza kuzorota haraka.
Siku ya Jumamosi, Ofisi ya Mambo ya Nje ilirudia wito kwa raia wa Uingereza kuondoka Lebanon - huku ikithibitisha kwamba maandalizi yalikuwa yanaendelea kusaidia na uhamishaji kutoka nchi hiyo ikiwa ni lazima.
Takriban raia 16,000 wa Uingereza wako Lebanon kwa sasa , Waziri wa Mambo ya Nje David Lammy aliliambia Baraza la Wawakilishi wiki iliyopita.
Mamia ya wanajeshi wametumwa Cyprus, ambako Uingereza tayari ina jeshi.
Wakati huo huo, nchini Uingereza, mamia ya wanajeshi zaidi wamepewa notisi - ikimaanisha kuwa wako tayari kutumwa katika eneo hilo ikiwa ni lazima. Uingereza tayari ina uwepo mkubwa wa kijeshi huko Cyprus.
Kituo cha RAF kilicho Akrotiri huenda kikawa kitovu cha safari zozote za angani, huku ndege za kivita za RAF Typhoon tayari zikiwa hapo.
Ndege hizo zilihusika katika ulinzi dhidi ya ndege isiyo na rubani ya Iran na shambulio la kombora dhidi ya Israel mwezi Aprili.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje mwishoni mwa juma ilisema wanajeshi wako katika harakati za kupeleka msaada wa kiutendaji kwa balozi za Uingereza katika eneo hilo.
Haikutaja idadi ya wanajeshi waliohusika.