Aliyempiga ngumi Waziri Mkuu wa Denmark afungwa jela
HABARI
Published on 08/08/2024

Mwanaume mmoja raia wa Poland amepatikana na hatia ya kumpiga ngumi Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen.

Mahakama ya Copenhagen ilimhukumu kifungo cha miezi minne jela, kufukuzwa nchini na kupigwa marufuku kuingia Denmark kwa miaka mitano.

Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 39, ambaye hakutajwa jina, aliimbia mahakama siku ya Jumanne kwamba alikuwa amelewa sana kukumbuka kilichotokea.

Bi Frederiksen alipata majeraha madogo alipopigwa ngumi begani wakati wa shambulio hilo katika uwanja mmoja mjini humo mwezi Juni.

Pamoja na shtaka la unyanyasaji dhidi ya mtumishi wa umma, mtu huyo pia alipatikana na hatia kwa makosa kadhaa ya ulaghai na utovu wa nidhamu unaohusiana na matukio mengine.

Baada ya kutumikia kifungo chake jela atafukuzwa nchini. Pia atalazimika kulipa gharama za kesi.

Bi Frederiksen hakutoa ushahidi katika kesi hiyo. Mshtakiwa alikana shtaka la kushambulia lakini alikiri mashtaka mengine.

Alisema alikuwa amekunywa pombe kupita kiasi ya kutoweza kukumbuka kilichotokea na kwamba alikuwa na "siku mbaya" alipokutana ana kwa ana na Bi Frederiksen.

Comments
Comment sent successfully!