Jeshi la Iran Revolutionary Guard Corps (IRGC) limeishutumu Israel kwa kumuua mkuu wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh kwa kutumia "kombora la masafa mafupi" lililorushwa kutoka nje ya nyumba yake ya kulala mjini Tehran.
Kikosi hicho kilisema kuwa kombora hilo lilikuwa na uzito wa kilo 7 (lbs 16) na lilisababisha "mlipuko mkubwa", na kuwaua Haniyeh na mlinzi wake.
Kiongozi huyo wa Hamas alikuwa katika mji mkuu wa Iran kwa ajili ya hafla ya kuapishwa kwa Rais Massoud Pezeshkian.
Kikosi hicho pia kilishutumu Marekani kwa kuunga mkono operesheni hiyo. Israel haijatoa tamko lolote kuhusu kifo cha Haniyeh.
Taarifa ya IRGC ni kinyume na ripoti katika vyombo vya habari vya Magharibi, ambavyo vimedokeza kuwa vilipuzi viliwekwa katika makazi ya Haniyeh ya Tehran na maofisa wa Israeli.