Muuaji wa watu wengi ambaye 'aliwawinda' watu weusi asema polisi walimtia moyo
HABARI
Published on 23/07/2024

Muuaji wa Afrika Kusini aliyepatikana na hatia ambaye aliwapiga risasi makumi ya wanaume weusi wakati wa ubaguzi wa rangi ameambia BBC kuwa polisi waliidhinisha ghasia zake. Louis van Schoor anasema wengine wanapaswa kushiriki lawama kwa mauaji aliyotekeleza kama mlinzi. Lakini katika kuzungumza na BBC Africa Eye katika kipindi cha miaka minne iliyopita, pia ameacha maelezo ya kutisha ambayo yanazua maswali mazito kuhusu kuachiliwa kwake mapema kutoka gerezani.

Kusimama katika chumba cha kulala cha muuaji, macho yako kwa kawaida hutazama maelezo.

Kitanda cha Van Schoor ni nadhifu kabisa - Blankenti yake imetandazwa vizuri sana inaonekana kana kwamba imepigwa pasi. Hewa ni nzito kwa harufu ya sigara, vijiti vyao vimerundikana juu kwenye kijibakuli cha majivu. Vipande vya karatasi vinaning'inia kutoka kwenye dari, vinapindana na nzi walionaswa na wanaokufa.

Anayejiita "Apartheid Killer" amepoteza meno. Afya yake inadhoofika. Kufuatia mshtuko wa moyo, miguu yake yote miwili ilikatwa hivi majuzi, na kumwacha kwenye kiti cha magurudumu, akiwa na makovu na maumivu makali. Wakati daktari wake wa upasuaji alipofanya utaratibu huu, Van Schoor aliomba kudungwa dawa ya kumfisha ganzi katika uti wa mgongo badala ya anesthesia yakawaida - ili aweze kuwatazama wakiondoa miguu yake.

"Nilikuwa na hamu," alisema, akicheka. "Niliwaona wakikata ... walikata mfupa."

Akiongea na Idhaa ya BBC World , Van Schoor alitaka kutushawishi kwamba "yeye sio jini kama wanavyosema watu". Maelezo yake kuhusu kuondolewa kwa miguu yake hayakusaidia sana kubadilisha msimamo wa wengi kumhusu .

Katika kipindi cha miaka mitatu katika miaka ya 1980 chini ya mfumo wa ubaguzi wa rangi nchini humo - ambao uliweka uongozi mkali uliowapa upendeleo Wazungu wa Afrika Kusini - Van Schoor aliwapiga risasi na kuwaua takriban watu 39.

Waathiiriwa wake wote walikuwa weusi. Mdogo alikuwa na umri wa miaka 12 tu. Mauaji hayo yalitokea Mashariki mwa London, mji ulioko katika eneo la Eastern Cape nchini Afrika Kusini.

Van Schoor alikuwa mlinzi wakati huo, akiwa na kandarasi ya kulinda hadi asilimia 70 ya biashara zinazomilikiwa na wazungu: migahawa, maduka, viwanda na shule. Kwa muda mrefu amedai kwamba kila mtu aliyemuua alikuwa "mhalifu" ambaye alimkamata akivunja majengo haya.

"Alikuwa kama muuaji wa kundi la sungusungu. Alikuwa mhusika kama 'Dirty Harry,” anasema Isa Jacobson, mwandishi wa habari na mtengenezaji wa filamu wa Afrika Kusini, ambaye ametumia miaka 20 kuchunguza kesi ya Van Schoor.

"Hawa walikuwa wavamizi ambao, katika visa vingi, walikuwa wamekata tamaa sana. Kupekua ndani ya mapipa, labda kuiba chakula… wahalifu wadogo.”

Mauaji yaliyotekelzwa na Van Schoor - wakati mwingine ya watu kadhaa katika usiku mmoja - yalizua hofu katika jamii ya watu weusi ya London Mashariki. Hadithi zilienea katika jiji kumhusu mtu mwenye ndevu - aliyepewa jina la utani "sharubu" katika lugha ya Xhosa - ambaye aliwafanya watu kutoweka usiku. Lakini risasi zake hazikupigwa kwa siri.

Kila mauaji kati ya 1986 na 1989 yaliripotiwa kwa polisi na Van Schoor mwenyewe. Lakini kuachiliwa kutoka jela kwa kiongozi aliyepinga ubaguzi wa rangi Nelson Mandela mwaka 1990 kuliashiria mwisho wa hali hii ya kutokujali. Mawimbi ya mabadiliko yalienea Afrika Kusini na, kufuatia shinikizo kutoka kwa wanaharakati na waandishi wa habari, mlinzi huyo alikamatwa mwaka wa 1991.

Kesi ya Van Schoor ilikuwa mojawapo ya kesi kubwa zaidi za mauaji katika historia ya Afrika Kusini, ikihusisha makumi ya mashahidi na maelfu ya kurasa za ushahidi wa kortini .

Hata hivyo, kesi dhidi yake iliporomoka kwa kiasi kikubwa mahakamani. Wakati wa kesi yake, vifaa vingi vya mfumo wa ubaguzi wa rangi vilikuwa bado vipo ndani ya mahakama. Licha ya kuua watu wasiopungua 39, alipatikana na hatia ya mauaji saba pekee.Alitumikia kifungo cha miaka 12 tu.

Mauaji yake mengine ya watu 32 bado yanaainishwa kama "mauaji yanayohalalishwa" na polisi. Sheria za zama za ubaguzi wa rangi ziliwapa watu haki ya kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wavamizi ikiwa walikataa kukamatwa au kukimbia mara tu walipokamatwa.

Van Schoor alitegemea sana utetezi huu kudumisha kutokuwa na hatia, akidai kuwa waathiriwa wake walikuwa wakikimbia wakati alipowaua.

TH
Maelezo ya picha,Louis van Schoor alionyesha mahali ambapo angefuatilia wavamizi

Uchunguzi wa BBC kuhusu Van Schoor ulichambua ushahidi uliotokana na matukio haya ya kupigwa risasi "yanayoweza kuhalalishwa", ikichunguza kwa kina ripoti za polisi zilizosahaulika kwa muda mrefu, uchunguzi wa maiti na taarifa za mashahidi.

Uchunguzi huo uliongozwa na Isa Jacobson, na ulihusisha miaka ya utafiti wa kumbukumbu katika miji mingi kote Eastern Cape. Faili muhimu zaidi zilitawanywa kati ya mamia ya masanduku, yaliyofichwa .

"Kiwango hiki kizima ni cha kushtua," alisema. "Inashangaza kwamba mahakama yoyote ya sheria inaweza kuruhusu hili kutokea."

Baadhi ya ushahidi wa kutisha zaidi Bi Jacobson alipata ni taarifa za mashahidi kutoka kwa watu ambao walijeruhiwa na Van Schoor, lakini wakanusurika. Maelezo haya yanapingana na hoja ya mlinzi kuwa walikuwa wakikimbia wakati anawapiga risasi.

Watu wengi walisema Van Schoor aliwapiga risasi wakiwa wameinua mikono juu, baada ya kujisalimisha. Wengine wanaelezea jinsi alivyokuwa akicheza nao, akiwauliza ikiwa wangependelea kukamatwa au kupigwa risasi - kabla ya kuwapiga risasi kifuani. Mwathiriwa mwingine alieleza kupigwa risasi tumboni, akiomba maji, kabla ya kupigwa teke kwenye jeraha lake na Van Schoor.

Mlinzi huyo alikuwa amejihami kwa bastola ya 9mm semi-otomatiki, mara kwa mara iliyokuwa na risasi ambazo husababisha milipuko mikali ya ndani wakati wa kuingia katika mwili wa mwathiriwa. Katika kisa kimoja, alifyatua risasi nane kwa mtu asiye na silaha.

Katika kesi ya kikatili sana mnamo tarehe 11 Julai 1988, Van Schoor alimpiga risasi mvulana wa miaka 14 ambaye alikuwa amevamia mgahawa akiomba msaada wa senti.

Mvulana huyo - ambaye hatujamtaja ili kulinda usiri wake - aliwaambia polisi kwamba alijificha kwenye choo alipomwona Van Schoor akiwa na bunduki yake. Anasema mlinzi alimuita nje, akamwambia asimame karibu na ukuta, kisha akampiga risasi mfululizo.

“Aliniambia nisimame, lakini sikuweza,” alisema mvulana huyo, katika ushuhuda wake uliorekodiwa. “Nikiwa nimelala alinipiga teke la mdomo. Alininyanyua na kuniegemeza kwenye meza kisha akanipiga risasi tena.”

Mvulana huyo alinusurika, lakini hakuaminiwa. Alishtakiwa kwa kuvamia jengo hilo. Vijana wengi weusi na wavulana ambao walitoa maelezo ya moja kwa moja ya kushambuliwa na kupigwa risasi na Van Schoor walikabiliwa na hatima kama hiyo.

Ushahidi kama huu ulisikilizwa wakati wa kesi ya Van Schoor, lakini hakimu aliwatupilia mbali mashahidi hao kama "wasio na ujuzi" na "wasioaminika". Hakuna kesi za jopo la wanasheria au waamuzi nchini Afrika Kusini kwa hivyo Maoni ya hakimu ni ya mwisho.

Wakati wa kesi ya Van Schoor, watu wengi wa jamii ya wazungu huko London Mashariki walimuunga mkono. Mfanyabiashara mmoja mjasiriamali alichapisha vibandiko vyenye picha za mlinzi huyo. Viliandikwa "Nampenda Louis", karibu na moyo uliojaa mashimo ya risasi.

"Kulikuwa na ubaguzi wa rangi katika mfumo wa sheria," anasema Patrick Goodenough, mwandishi wa habari wa Afrika Kusini ambaye aliongoza uchunguzi wa miaka ya 1980 kuhusu Van Schoor. Pia alihudhuria kesi yake.

"Msaada kwa ajili yake ulikuwa mkubwa ... Hangeweza kukwepa sehemu ya kile alichopata bila msaada."

Hakuna sheria ya vikwazo kwa mauaji au jaribio la mauaji nchini Afrika Kusini. Kinadharia, hakuna chochote kinachowazuia polisi kufungua tena kesi ya Van Schoor na kutathmini upya ukatili huu "unaoweza kuhalalishwa".

"Louis van Schoor kimsingi alikuwa akitoka nje na kuua watu kama mchezo," anasema Dominic Jones, mwandishi wa habari ambaye alisaidia kuongeza ufahamu wa mauaji ya mlinzi huyo katika miaka ya 1980.

Baadhi ya matokeo ya kushtua kutoka kwa uchunguzi wa BBC yalitokana na mahojiano na Van Schoor mwenyewe, ambayo yalipendekeza kwa nguvu kuwa alipata msisimko kutokana na shughuli zake.

"Kila usiku ni 'adventure' mpya, ikiwa unataka kuiweka kwa njia hiyo," aliiambia BBC.

TH
Maelezo ya picha,Mwanahabari Isa Jacobson ametumia miaka mingi kupitia rekodi za umma kuchunguza kesi ya Louis van Schoor

Biashara nyingi alizozilinda ziliweka kengele za kimyakimya. Wakati mtu aliingia, Van Schoor angepokea arifa ambayo ilimruhusu kumshtukiza mvamizi - na kutambua ni wapi walikuwa ndani ya jengo hilo. Na kila mara alienda peke yake.

“Nilikuwa bila viatu. Kulikuwa na kimya. Huna viatu vyako vinavyopiga kelele kwenye vigae na vitu vingine,” alisema.

Hangewasha taa kamwe. Badala yake, alitegemea hisi yake ya kunusa.

"Mtu akifanya uvamizi katika jengo, adrenaline hutoa harufu. Na unaweza kunusa hiyo, "alisema.

Van Schoor anadai hakuwahi kutoka nje "kwa nia ya kuua watu weusi" na anasema yeye si mbaguzi wa rangi. Lakini anakiri alifurahia 'msisimko' wa kuwanyemelea gizani .

Kabla ya kuwa mlinzi, Van Schoor alikuwa mwanachama wa jeshi la polisi la London Mashariki kwa miaka 12. Alikuwa akikabiliana na kile anachokiita "mbwa washambuliaji", ambao aliwatumia kuwafuatilia na kuwakamata waandamanaji na wahalifu - karibu wote walikuwa weusi.

Alilinganisha hii na "uwindaji, lakini wa aina tofauti".

TH

CHANZO CHA PICHA,LOUIS VAN SCHOOR

Tetinene “Joe” Jordan, mwanaharakati wa zamani wa kupinga ubaguzi wa rangi ambaye alikuwa akiendesha shughuli zake huko London Mashariki wakati wa mauaji ya Van Schoor, anakumbuka hili vyema.

"Alikuwa akiwinda, akiwinda hasa watu weusi," asema.

Van Schoor anakanusha vikali kuwa yeye ni "muuaji wa kiholela" na anaamini kila kitu alichokifanya kilikuwa "ndani ya sheria". Iwapo watu wanahisi kuhuzunishwa na mauaji yake, anasema wanapaswa kulaumu polisi wa Afrika Kusini.

Anasema polisi hawakuwahi kumkosoa wala kumuonya, bali walimuunga mkono na kumtia moyo.

"Kila afisa katika London Mashariki alijua kinachoendelea ... maafisa wote wa polisi walijua," alisema. "Si mara moja mtu yeyote alisema 'Hey Louis, umevuka mipaka au unapaswa kupunguza au chochote' ... wote walijua kinachoendelea."

Katika rekodi za polisi zilizohifadhiwa katika hifadhi za umma, Bi Jacobson alipata visa vya mauaji ambapo maafisa walikuwa wamekuwepo wakati wa ufyatuaji risasi. Hakuna wakati walionekana kumhoji Van Schoor kama mshukiwa.

Katika matukio mengi, polisi walishindwa kuchukua picha za marehemu kwenye matukio ya kupigwa risasi na kushindwa kukusanya ushahidi muhimu wa kiuchunguzi, kama vile maganda ya risasi. Van Schoor mara nyingi alikuwa shahidi pekee wa kupigwa risasi alikofanya, kwa hivyo ushahidi huu ungeweza kuwa muhimu kwa kuamua nini kilikuwa kimetokea katika kila kesi.

"Haya yalikuwa mambo ya siri... Aliungwa mkono na maafisa wa polisi kutoka vyeo vya chini na vyeo vya juu," alisema Bw Goodenough.

“Hawangefanya uchunguzi. Wangeketi naye na kuvuta sigara huku wakipiga soga, miili yao waathiriwa ikiwa imelala karibu.”

ambapo Van Schoor alifyatua risasi - lakini polisi na wafanyabiashara waliomwajiri, jamii nzima ilihusika katika mauaji ambayo yalifanyika London Mashariki.

"Van Schoor alikuwa muuaji sugu kwa sababu kulikuwa na jamii iliyomruhusu kuwa muuaji," asema Bi Jacobson.

Kwa jamaa za waathiriwa wa Van Schoor, uhuru wake, na kushindwa kwa serikali kuchunguza kwa kina mauaji aliyotekeleza , ni chanzo cha maumivu kila wakati. Wengine hawakupata tena miili ya wapendwa wao.

"Inaonekana kama tumekwama katika awamu hii ya kuvunjika moyo, kuwa na hasira," anasema Marlene Mvumbi, ambaye kaka yake, Edward, aliuawa na Van Schoor mwaka 1987. Mwili wake ulitupwa kwenye kaburi lisilojulikana na mamlaka bila idhini ya familia. .

"Watu wengi bado wamepotea na hata kwenye makaburi ... hakuna tamati kwa awamu hii ya majonzi."

Kesi ya Van Schoor ilikuwa kabla ya Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Afrika Kusini ya 1995, ambayo ilitoa fidia kwa waathiriwa wengi wa uhalifu wa enzi za ubaguzi wa rangi.

Sharlene Crage, mwanaharakati wa zamani ambaye anatekeleza jukumu muhimu katika kushinikiza mamlaka ya Afrika Kusini kumfungulia mashitaka Van Schoor, amekasirishwa kwamba aliwahi kuruhusiwa kuwa huru.

"Ni upotovu wa kutisha wa haki," alisema. "Hakuna sababu kesi yake isifunguliwe tena."

TH
Maelezo ya picha,Louis van Schoor alikiri alipata kuwafuatilia wavamizi kwa msisimko

Van Schoor alihukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka 90 jela mwishoni mwa kesi yake mwaka 1992, lakini hakimu alimruhusu kutumikia kila kifungo kwa wakati mmoja. Aliachiliwa kwa msamaha mnamo 2004.

Kuachiliwa mapema kwa wauaji wa enzi za ubaguzi wa rangi kutoka gerezani imekuwa suala la utata nchini Afrika Kusini.

Mnamo 2022, kulikuwa na maandamano huko Johannesburg kuhusu kuachiliwa kwa Janusz Walus, ambaye alimuua mwanasiasa anayepinga ubaguzi wa rangi Chris Hani . Miaka michache hapo awali, Eugene de Kock, anayesimamia kikosi cha mauaji kilichohusika na utekaji nyara, utesaji na mauaji ya makumi ya wanaharakati weusi pia aliachiliwa.

Siku hizi, Van Schoor hutumia muda wake mwingi kutazama raga, kuvuta sigara na kucheza na kipenzi chake ,mbwa aina yacha rottweiler, Brutus. Anasema hana kumbukumbu ya mauaji yake mengi.

Baadhi ya ripoti zimesema, bila uthibitisho, kwamba aliwapiga risasi takriban watu 100. Van Schoor anakanusha hili, lakini anakubali idadi ya watu aliyowapiga risasi inaweza kuzidi idadi iliyorekodiwa ya 39.

“Kiukweli sijui nilipiga risasi watu wangapi. Wengine wanasema zaidi ya 100, wengine 40… Wacha tuseme kwa ajili ya hoja nilipiga watu 50,” alituambia.

Anasema anajivunia vitendo vyake vya zamani.

"Sijisikii kuwa na hatia yoyote," alisema. "Sina majuto ndani."

BBC iliwasiliana na polisi wa Afrika Kusini ili kutoa maoni yao, lakini hawakujibu. Mamlaka haijatoa maelezo kwa nini mauaji yaliyotekelezwa na Van Schoor hayajatathminiwa tena katika zama za baada ya ubaguzi wa rangi.

"Kuna uchungu mwingi, na kwa sasa sijisikii kwamba kuna yanayofanywa ili tupone," anasema Marlene Mvumbi.

“Sio wale tu waliouawa na Van Schoor. Wale ambao wana visa kama hivyo vya mauaji ya utawala wa kibaguzi."

Comments
Comment sent successfully!